Uchumi
wa Tanzania umekuwa ukizalisha ajira chache kila siku. Hii imekuwa
ikifanya vijana wengi wanaohitimu vyuoni kubaki wakizunguka na bahasha
kila kona kusaka ajira.
Takwimu
kutoka ofisi ya takwimu ya taifa zinaonyesha kuwa mwaka 2014 taifa
lilizalisha nafasi za ajira 282,382 tu ukilinganisha na mahitaji ya
zaidi ya wahitimu 400,000 wanaomaliza vyuo kila mwaka.
Hii
inaonyesha dhahiri kuwa Tanzania kama nchi inahitaji kuweka nguvu za
ziada katika kuhakikisha kuwa nafasi zaidi za ajira zinatengenezwa.
Pengine njia pekee inayoweza kutumiwa kupunguza tatizo hili au hata kulimaliza kabisa ni kupitia ajira binafsi (Ujasiriamali).
Pamoja
na kuwa ujasiriamali unaweza kuwa suluhisho la ajira nchini, vijana
wengi wameshindwa kabisa kufanya ujasiriamali kutokana na kukosa elimu
sahihi. Kwa bahati mbaya sana mfumo wetu wa elimu haumsaidii sana
muhitimu kupata stadi za ujasiriamali.
Katika
vipaumbele vyake, Rais John Magufuli anasisitiza sana Tanzania ya
viwanda, lakini hili litatokea tu kama vijana wa kitanzania watapatiwa
elimu ya ujasiriamali.
Sehemu
hii itakuwa ikiwapatia makala mbalimbali za ujasiriamali… tutajifunza
jinsi ya kuanzisha biashara, jinsi ya kuendeleza biashara yako na namna
ya kupata fedha.
Leo tutaanza kujifunza mambo ya msingi katika kuanzisha biashara.
Biashara
yoyote huanza na wazo, ila wazo pekee halitoshi, linahitaji kufanyiwa
kazi. Hapo ndipo watu wengi huweza kuanza kujisikia kuzidiwa. Si ajabu
kuona mtu anakatishwa tamaa kwa kutizama msururu wa mambo yanayohitajika
ili kuanzisha biashara, lakini pia kuanzisha biashara ni rahisi kuliko
unavyodhani. Kama ilivyo katika lengo lolote kubwa, ukianza kwa
kutengeneza malengo madogo madogo ya kutekeleza utaweza kufanya mambo
yote muhimu katika kuanzisha biashara.
Kuanzisha
na kuendesha biashara inahitaji msukumo, nia na kipaji. Inahitaji pia
utafiti na mipango. Kama ilivyo kwenye mchezo wa drafti, mafanikio
kwenye biashara ndogo huanza na maamuzi sahihi katika hatua za mwanzoni.
Ikumbukwe pia hapa kuwa pamoja na kwamba makosa madogomadogo ya
mwanzoni yanaweza yasiue biashara yako, inahitaji ujuzi, nidhamu, na
bidii kuyasahihisha.
Ili
kuboresha uwezekano wa kufanikiwa, unapaswa kutenga muda wa
kujichunguza na kutathmini malengo yako kibiashara na malengo binafsi.
Tumia taarifa hiyo kutengeneza kwa umakini mkubwa mpango wa biashara
ambao utakuwezesha kufikia malengo yako.
Mchakato
wa kuandaa mchanganuo wa biashara utakuchochea kufikiria hata baadhi ya
mambo ambayo usingekumbuka kuyafikiria katika hali ya kawaida.
Mchanganuo wako utakuwa zana muhimu sana unapopambana kutafuta fedha kwa
ajili ya biashara yako. Mchanganuo huo pia unaweza kutumika kama kigezo
cha kila mara kufuatilia/ kupima mafanikio ya biashara yako.
Yako mambo kadhaa yanayohitajika katika biashara yoyote.
Jambo
la kwanza kabla ya kuanzisha biashara ni kuwa unatakiwa ujiulize sababu
za wewe kutaka kuingia kwenye biashara. Sababu zilizozoeleka za kuanza
biashara ni:
- Unataka kujiongoza mwenyewe.
- Unataka uhuru wa kifedha.
- Unataka uhuru wa kutumia ubunifu wako.
- Unataka kutumia kikamilifu ujuzi na ufahamu wako
Jambo la pili ni kuamua biashara ipi inakufaa? Ili kufahamu ni biashara ipi inakufaa, jiulize maswali yafuatayo:
- Ninapenda kutumiaje muda wangu?
- Nimejifunza au kusomea ujuzi gani?
- Watu wengine wanazungumzia ubora wangu kwenye mambo gani?
- Nina muda kiasi gani kuendesha biashara kwa ufanisi?
- Katika mambo ninayopendelea yapo ambayo yanaweza yakawa fursa ya biashara?
- Biashara yangu itahudumia sehemu/ kundi gani katika soko?
- Je? Wazo langu linatekelezeka na litakidhi hitaji katika soko?
- Ushindani nilionao ni upi? Nami nina uwezo gani katika ushindani?
- Biashara yangu ina manufaa gani kuzidi zingine zilizopo?
- Je? Naweza kutoa huduma zenye ubora zaidi?
- Je? Naweza kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa/ huduma zangu?
Ukishapata
majibu ya maswali hayo hapo juu ni wazi kuwa utakuwa ulishaanza kujua
ni biashara gani unaweza kuianzisha. Lakini pia unatakiwa ujiulize
maswali haya hapa ili kuwa na uhakika na biashara ambayo utaifanya.
- Ninakusudia kuanzisha Biashara gani?
- Nitauza bidhaa gani au nitatoa huduma gani? Biashara nitafanyia eneo gani?
- Nitatumia ujuzi na uzoefu gani kwenye biashara?
- Biashara yangu itakuwa na muundo gani kisheria?
- Niiite biashara yangu jina gani?
- Nitatumua vifaa gani, na nitakuwa na mahitaji gani?
- Nahitaji bima ya aina gani?
- Nahitaji fedha kiasi gani?
- Nina rasilimali zipi?
- Nitajilipaje?
Majibu
yako yatasaidia kutengeneza mpango makini, uliofanyiwa utafiti wa
kutosha, ambao utautumia kama ramani ya kuelekeza kila hatua katika
utekelezaji wa biashara na hata kupata mtaji.
Unapoanzisha
biashara yoyote, mojawapo ya maamuzi muhimu sana ya kufanya ni uchaguzi
wa muundo wa hiyo biashara. Mambo yanayozingatiwa katika kuchagua
muundo wa biashara ni pamoja na:
- Masharti ya kisheria
- Uwajibikaji wa wamiliki kwa madeni ya biashara
- Aina ya shughuli za biashara
- Mgawanyo wa mapato
- Mahitaji ya mtaji
- Idadi ya wafanyakazi na utawala
- Manufaa na hasara za kihasibu/ kikodi
- Urefu wa mzunguko wa biashara
Tuishie hapa kwa leo, wiki ijayo tutajifunza aina za biashara.
0 Comments